Kaimu mkuu wa shule ya sekondari Unyahati jimbo la Singida, Mboya David akiwa ofisini kwake akitekeleza majukumu yake.
Meza ya mkuu wa shule ya sekondari ya Unyahati jimbo la Singida mashariki linaloshikiliwa na CHADEMA.
Kutokana na ofisi ya mkuu wa shule ya sekondari ya Unyahati jimbo la Singida mashariki kutokuwa na kabati za kutunzia nyaraka imelazimika kutumia viti vya plastiki kutunza nyaraka mbalimbali.
Mwalimu Mboya David kaimu mkuu wa shule ya sekondari ya kata Unyahati jimbo la Singida mashariki ambalo mbunge wake ni Tundu Lissu aliyejipatia umaarufu kwa hoja zake bugeni, akikagua choo cha nyasi chenye matundu nane kinachotumiwa na wanafunzi wavulana 173 wa shule hiyo.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Unyahati jimbo la Singida mashariki,wanaketi kwenye viti vya plastiki na kuandikia kwenye mapaja yao kutokana na kukosa madawati.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Ikungi
SHULE ya sekondari ya Unyahati iliyopo kijijini kwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA),Tundu Lissu inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ya uhaba mkubwa wa vyoo hali inayochangia wanafunzi kutumia choo cha nyasi.
Kaimu mkuu wa shule hiyo, Mbaya David amesema kuwa kutokana na wazazi/walezi wa jimbo hilo kuwa kwenye mgomo wa kuchangia wala kushiriki miradi yao ya maendeleo mbalimbali ikiwemo ya sekta ya elimu,hali hiyo imechangia mwaka jana walimu wa shule hiyo na wanafunzi kuchimba choo ambacho wakati wa masika, kilidumbukia kutokana na kuwa chini ya kiwango.
“Jimbo hili ukitamka jambo la michango au watu kushiriki utekelezaji wa miradi, huwezi kueleweka.Wazazi/walezi wameishaambiwa kuwa serikali ina fedha nyingi ya kugharamia miradi yote na wao kama wananchi, hawahusika kabisa na jukumu hilo”amesema.
Kwa hali hiyo, amesema ili shule isije ikafungwa kwa kukosa choo, shule imeamua ijenge choo cha muda ambacho ni cha nyasi.
David amesema pamoja na changamoto ya choo zipo zingine ikiwemo ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kutumia viti vya plastiki darasani na hali hiyo inachangia waandikie juu ya mapaja yao.
Kaimu mkuu huyo wa shule, alitaja changamoto zingine kuwa shule hiyo haina kabisa nyumba za walimu kitendo kinachochangia wapange katika kijiji cha Ikungi kilichopo umbali wa kilomita nne. Hali hiyo inachangia mwalimu kutembea kilomita nane kwa siku kwenda shuleni.
“Hapa kwetu hatuna jengo la utawala jambo linalosababisha tubadilishe matumizi ya vyumba viwili vya madarasa na kuwa ofisi za walimu.Tunakabiliwa na upungufu mkumbwa wa samani ikiwemo makabati kitendo kinachotulazimisha kutumia viti vya plasitiki kuhifadhia nyaraka mbalimbali”, amesema Divid.
Kuhusu vyumba vitatu vya maabara, David amesema kuwa hali ni mbaya mno kwa sababu hata kutenga eneo lenyewe la kujenga vyumba hivyo halijatengwa.
Kwa mujibu wa uongozi wa shule hiyo ingawa shule hiyo imejengwa kijijini kwa Tundu Lissu, lakini toka ianzishwe miaka saba iliyopita mbunge huyo hajaweza kutembelea shuleni hapo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana shuleni hapo, hakuna ndugu wa karibu na mbunge Tundu anayesoma shuleni hapo. Hata hivyo mbunge Tundu Lissu, amealikwa kwenye harambee ya kuchangia maendeleo ya shule ya kijijini kwao.
Juhudi za kumpata Tundu aweze kuzungumzia changamoto za shule hiyo zilikwama baada ya kumtumia ujumbe kwa njia ya simu hakujibu na alipopigiwa, hakupokea.
Hivi karibuni mkuu wa wilaya ya Ikungi, Manju Msambya amesema kuwa kabla ya mwaka 2010 wakazi wa jimbo hilo walikuwa mstari wa mbele katika kujenga shule za sekondari za kata na kata mbili zilijenga sekondari mbili. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 mambo yalibadilika baada wananchi kukatazwa kuchangia maendeleo yao.